LEO Alhamisi ni Azam na Simba kwenye Uwanja wa Mkapa. Kaimu kocha wa Simba, Juma Mgunda amesema wachezaji wamecheza mechi ngumu ambayo walitumia nguvu nyingi lakini amejipanga kuhakikisha anapata pointi na mabao zaidi ya mawili huku straika wa Azam, Idris Mbombo akisema wamepania. Azam wao nao wanaingia wakitaka kupata ushindi baada ya mechi yao iliyopita dhidi ya KMC kupoteza kwa mabao 2-1. Mgunda alisema; “Natambua wachezaji wangu wametoka kucheza dakika 90 ngumu dhidi ya Yanga na wametumia nguvu nyingi, tunakutana na Azam FC ambayo pia ni timu nzuri nina imani na jeshi langu kwasababu wako vizuri kwenye utimamu wa mwili, naamini watafanya vizuri.” “Ugumu utakuwepo kwa sababu tunakutana na timu nzuri na shindani lakini kwa upande wangu nimewaandaa vizuri wachezaji wangu na wao wanatambua nini tunakitaka ili kuendelea kuongoza msimamo, sio pointi tatu tu pia tunahitaji idadi kubwa ya mabao ambayo yataongeza idadi ya ushindani,” alisema. Alisema wanaongoza ligi kwa utofauti wa mabao ya kufungwa na wanaokimbizana nao hivyo kwenye mchezo huo anatamani kuona timu yake inapata matokeo mazuri dhidi ya wapinzani wao pamoja na kupata idadi nzuri ya mabao ili kuongeza ushindani kutoka kwa wanaowafukuza. MBOMBO APANIA Kwa upande wa mshambuliaji wa Azam FC, Mkongomani Idris Mbombo alisema licha ya kiwango kizuri kutoka kwa wapinzani wao Simba, ila haliwapi shida kupambana nao kwani imani yao kubwa ni kuhakikisha wanaibuka na ushindi watakapokutana. Mbombo alisema; “Hatujaanza vibaya sana wala vizuri kwa sababu bado ni mapema, tunahitaji kurejesha morali ya kupambana hasa baada ya kupoteza mchezo wetu wa mwisho na KMC, licha ya ushindani wa ligi uliopo,” alisema na kuongeza; “Mabadiliko ya benchi la ufundi hayawezi kutuathiri sana kwa sababu sisi ni wachezaji wakubwa tunaojielewa, hivyo jukumu letu ni kutimiza kile ambacho tunatakiwa kukifanya kwa niaba ya mashabiki na viongozi wetu.” Azam inaingia kwenye mchezo huu ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa mabao 2-1 na KMC Oktoba 21 huku Simba wao ikifungana bao 1-1 na watani zao Yanga iliyopigwa uwanja huo Oktoba 23. Katika michezo saba ambayo Azam imecheza imeshinda mitatu, sare mbili na kupoteza miwili ikishika nafasi ya sita na pointi 11 huku Simba ambayo ni kinara imecheza mechi sita, ikishinda minne, sare mbili na kukusanya pointi 14. Mchezo wa mwisho kati ya timu hizi uliopigwa katika Uwanja wa Mkapa Januari 1, mwaka huu, Azam FC ilifungwa mabao 2-1, mabao ya Simba yakifungwa na Sadio Kanoute na Pape Sakho wakati lile la Azam lilifungwa na Mzambia, Rodgers Kola. Azam inaingia kwenye mchezo huu ikiwa na rekodi mbovu dhidi ya wapinzani wao kwani mara ya mwisho kushinda kwenye Ligi Kuu Bara ilikuwa Januari 28, 2017, iliposhinda bao 1-0 lililofungwa na John Bocco anayeichezea Simba kwa sasa.
The post Mgunda: Azam wapigwe nyingi, Mbombo acheka, amjibu appeared first on soka letu.
Via soka letu https://ift.tt/0tyXhQ8
Comments
Post a Comment