KAZI haijaisha. Hii ni wikiendi muhimu kwa Tanzania Bara na Visiwani ambapo timu nne zinawania kufuzu makundi ya Afrika. Simba ilishinda ugenini, lakini kazi haijamalizika hadi itakapozitumia dakika 90 za nyumbani kuhakikisha wanaing’oa Primeiro de Agosto ya Angola. Hali ipo pia kwa Yanga. Kutoka sare ya 1-1 nyumbani, haina maana kazi imeisha. Bado wana dakika nyingine 90 za kupindua meza dhidi ya Al Hilal ya Sudan wanaporudiana nao kesho mjini Khartoum. Hata kwa Azam FC, licha ya kuchezea kichapo cha mabao 3-0 ugenini mbele ya Al Akhdar ya Libya, haina maana imeshang’oka michuano. Bado ina turufu ya mwisho ikirudiana nao nyumbani kesho katika mechi ya raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika, kwani ikipata ushindi wa 3-0, ngoma itaenda kwenye matuta na kama itavuka idadi hiyo itaenda kwenye play-off kuwania kucheza makundi kwa mara ya kwanza kwenye ushiriki wao wa michuano ya CAF. Kadhalika kwa wawakilishi wengine wa Tanzania kutokea visiwani Zanzibar, Kipanga FC suluhu ya nyumbani dhidi ya mabingwa wa zamani wa Afrika, Club Africain ya Tunisia, haina maana tayari imeshatangulia play-off. Hapana ni lazima ipambane leo ugenini ili kupata angalau sare yoyote ya mabao iweke historia ya kufuzu play-off baada ya muda mrefu wa timu za visiwa hivyo kuwa wanyonge. Ndio, wikiendi hii ni mwisho wa yote kwa klabu nne za Tanzania, zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika. Yanga na Simba zenyewe zinashuka uwanjani kesho ili kutafuta nafasi ya kutinga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati, Azam na Kipanga zinazocheza pia kesho nazo zikiwania kufuzu hatua inayofuata ya play-off ya Kombe la Shirikisho ili kusaka tiketi ya makundi ya michuano hiyo. HALI ILIVYO Kwa upande wa Simba inayonolewa na makocha wazawa, mambo sio magumu sana kulinganisha na wawakilishi wengine, hii ikitokana na ushindi mnono wa mabao 3-1 ugenini mjini Luanda, Angola wikiendi iliyopita kuitanguliza mguu mmoja kwenye makundi. Simba itakayoshuka uwanjani kesho saa 10:00 jioni, itapaswa kulazimisha sare ya aina yoyote ili kujihakikishia inaenda makundi kwa mara ya tano katika misimu sita ya michuano ya Afrika. Hazina ya ushindi wa ugenini unaibeba, japo bado haipaswi kuchukulia poa kwa kurejea kilichowakuta msimu uliopita dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana. Kwa waliosahau ni kwamba Simba ilishinda ugenini kwa mabao 2-0 na kuamini kazi imeisha kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kuja kuduwaza nyumbani kwa kucharazwa mabao 3-1, ikitangulia kupata bao lililofungwa a Larry Bwalya aliyepo Amazulu ya Afrika Kusini kwa sasa. Wageni walicharuka na kurudisha bao hilo kabla ya kuongeza mengine mawili na kufanya matoke ya jumla baina ya timu hizo kuwa 3-3 na Simba kutolewa kwa bao la ugenini na kuangukia kwenye play-off ya Kombe la Shirikisho na huko ikafanya kweli na kufanikiwa kusonga mbele hadi robo fainali. Kocha Mgunda na vijana wake kesho wanatakiwa tu kuhakikisha wanashuka uwanjani bila kujiamini kupita kiasi na kuwadharau wapinzani wao, ili wasije wakahjaribu furaha waliyonayo mashabiki wao tangu timu iwe chini ya kocha huyo aliyenyakuliwa kutoka Coastal Union kuziba nafasi ya Zoran Maki aliyetimkia Al Ittihad ya Misri. Agosto ina wachezaji wasumbufu na wenye kasi, hivyo safu ya ulinzi ya Simba ni lazima iwe makini na wachezaji kama John Mano, Dago Tshibamba aliyefunga bao la kufutia machozi mjini Luanda pamoja na Vidinho. Kocha Mgunda hana kazi kubwa ya kubadilisha kikosi chake kwenye mchezo huo, luicha ya Peter Banda kurudi kutoka kwenye majeruhi, ambapo anaweza kuanzishwa sehemu ya Denis Kibu ambaye amekuwa hana utulivu anapokuwa na mpira na kutumia nafasi zinazotengenezwa kusaka mabao. Rekodi zinaonyesha Simba imekuwa ikitamba nyumbani na katika mechi 10 zilizopita za Uwanja wa nyumbani imepoteza moja tu dhidi ya Jwaneng Galaxy kitu kinachowapa mzuka mashabiki wa klabu hiyo wakiamini kesho wanavuka salama kwenda makundi baada ya mwaka 2003, 2018, 2018-2019, 2020-2021 katika Ligi ya Mabingwa na msimu uliopita ilicheza Kombe la Shirikisho la kuvuna hadi robo fainali kabla ya kuzimwa na Orlando Pirates ya Afrika Kusini. KAZI IPO HUKU Yanga iliyoondoka alfajiri ya leo kwenda Khartoum ndiyo yenye kazi kubwa kulingana na rekodi ilizonazo wenyeji wao kwenye mechi za nyumbani. Sare ya 1-1 nyumbani iliiweka Yanga kwenye nafasi ngumu ya kupindua meza, japo kwenye soka lolote linaweza kutokea, lakini ni ukweli kocha Nasreddine Nabi na vijana wake wana kazi kubwa ya kuonyesha ukubwa wao kwenye soka la Afrika kwa kubadilisha matokeo ikiwa ugenini. Uwepo wa nyota wote muhimu wa timu hiyo akiwamo kipa Diarra Djigui, kinara wa mabao wa Afrika kwa sasa Fiston Mayele, Stephane Aziz KI, Bernard Morrison, Feisal Salum, Yannick Bangala na wengine ni wazi inampa nafasi Nabi kujipanga jeshi lake ili kumduwaza Florent Ibenge wa Al Hilal. Ni mechi ya hamsini kwa hamsini hadi sasa kwani kwenye mechi iliyopita kila timu ilikuwa na nafasi ya kutoka na ushindi, lakini umakini mdogo wa washambuliaji wa timu zote na uimara wa makipa wa timu hizo uliufanya mchezo umalizike kwa sare hiyo iliyowanufaisha zaidi Al Hilal. Yanga inapaswa kushuka uwanjani kwa akili ya kutafuta bao la mapema ili kuwachanganya wapinzani wao ambao kucheza kwao usiku hutumia kama silaha ya kuwavuruga wageni kutokna na mashabiki wao walivyo na mizuka na vurugu hasa wanapitaka timu yao ipate ushindi. Rekodi zinaonyesha Al Hilal huwa inataabika sana kwa Yanga katika mechi ilizowahi kukutana kwenye michuano ya CAF na hata ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kagame Cup), lakini bado Yanga inapaswa kutafuta mabao ugenini ili yawabebe na kwenda makundi. Mara ya mwisho kwa Yanga kucheza makundi ya Ligi ya Mabingwa ilikuwa ni mwaka 1998 ikiwa ndio klabu ya kwanza ya Tanzania kufanya hivyo kipindi hicho tangu michuano hiyo ilipobadilishwa kutoka Klabu Bingwa Afrika mwaka 1997. Yanga imecheza pia makundi ya Shirikisho 2016 na 2018. Hivyo ni wazi mastaa wa timu hiyo wana kazi kubwa na wanajua wazi mapema kwamba wana mzigo mzito wa kutuliza mashabiki wao ambao hawana amani wala furaha tangu sare ya wikiendi iliyopita kutokana na ukweli walikuwa na matarajio makubwa kwenye mchezo huo wa kwanza. Kocha Nabi na baadhi ya nyota wake wameshatoa kauli za matumaini kwamba wanaenda kupindua meza na ni wajibu wao kutekeleza kwa vitendo kauli hiyo, la sivyo watapata aibu ikizingatiwa msimu huu imefanya usajili mzuri uliokuwa ukitajwa wenye lengo la kuibeba timu michuano ya Afrika. KIPANGA IJIPANGE Rekodi zinaonyesha hakuna timu ya Zanzibar iliyowahi kufanya makubwa kwenye michuano ya CAF tangu ilivyotamba Malindi ya Mohammed Naushad ambayo ilifika robo fainali na nusu fainali za michuano tofauti ya CAF ikiwamo Kombe la CAF na Kombe la Washindi Afrika. Timu za Zanzibar zimekuwa ikipasuka mabao mengi ugenini, kitu ambacho, Kipanga iliyo na faida ya suluhu ya nyumbani inapaswa kwenda Tunisia ikiwa na akili hiyo ya kupambana ili kuweka heshima baada ya kurejea michuano ya Afrika. Pia kuepuka aibu ya kutolewa kwa aibu katika michuano hiyo wakati wao ndio waliobeba tumaini la Zanzibar kwa sasa. Club Africain ina rekodi nzuri nyumbani, kitu kitakachoipa wakati mgumu Kipanga kuhakikisha inakomaa na kupata sare yoyote ya mabao ili isonge hatua inayofuata ili kuitafuta tiketi ya makundi ya Kombe la Shirikisho. Mechi ya Kipanga itapigwa kuanzia saa 12:00 jioni. AZAM INAWEZEKANA Azam itashuka uwanjani kesho saa 1:00 usiku kwa mechi yao ya Al Akhdar huku ikiwa na mlima mzito wa kipigo cha mabao 3-0, lakini bado haiwafanyi matajiri hao kukata tamaa. Kuanzia uongozi wa timu hiyo chini ya Mtendaji Mkuu, Abdulkarim Amin ‘Popat’, wachezaji na makocha wa Azam wamewatoa hofu mashabiki kwa kuwaambia watapindua mchezo huo kwa namna walivyojipanga. Inawezakana kuonekana ni ngumu, lakini kama Walibya walishinda kwao basi hata Azam ina nafasi ya kufanya hivyo nyumbani na kuandika historia. Nyota wa timu hiyo wanapaswa kucheza kwa umakini ili kutoruhusu wageni kupata bao na pia kuwadhibiti washambuliaji wa Al Akhdar ambao wana kasi na wajanja sana wanapoingia kwenye eneo la adui kama ilivyotokea kwenye mchezo wa kwanza. Kipre Junior, Tape Edinho, Prince Dube, James Amaninko, Isah Ndala na wengine wana kazi ya kuonyesha ukubwa wao kwenye mchezo huo kwa kuivusha timu hiyo kwenda hatua inayofuata. Hautakuwa mchezo mwepesi, lakini lolote linawekazana kama alivyosema kocha Denis Lavagne kuwa Azam ina dakika 90 za kupindua meza ikiwa nyumbani. MAKOCHA, MASTAA WAFUNGUKA Kocha Nabi wa Yanga, Juma Mgunda wa Simba, Lavagne wa Azam na kocha msaidizi wa Kipanga, Khamis Hassan kila mmoja kwa wakati wake alisema wameandaa timu zao kupata matokeo mazuri kwenye mechi hizo za marudiano ili kusonga mbele. Hassan anasema suluhu ya nyumbani haijawapa uhakika wa kupenya mbele ya Watunisia, ila wamekaa chini na kutathmini mchezo uliopita na kurekebisha makosa ili mechi ya kesho iwe nyepesi. “Hatujamaliza kazi, tuna dakika 90 za ugenini, tumerekebisha makosa na kwenda kupambana ili kuona tunavuka salama, muhimu mashabiki watuombee dua njema tupata matokeo mazuri,” alisema Kocha Hassan, wakati Lavagne alisema mechi ya kesho watashuka wakiwa na kiu ya kupindua meza kwani kama wenzao walishinda nyumbani hata wao wana nafasi ya kufanya vizuri Chamazi. Mgunda alisema licha ya kuonekana kama kazi imeisha kwao, lakini ukweli bado kuna kibarua kigumu kwa kutambua hata Waangola wamefanya tathmini ya walivyopoteza na wamekuja Dar wakiwa hawana cha kupoteza, hivyo kuufanya mchezo huo kuwa mgumu zaidi. “Peter Banda karejea na tumejipanga kumalizia kazi iliyobaki, kwani mechi haijaisha hadi dakika 90 zitakapotamatika Kwa Mkapa, tunatarajia mechi itakuwa ngumu na tutawaheshimu wapinzani ili tuendelee kuwapa raha mashabiki na pia kuona Simba inaenda makundi ikiwa ndio lengo la kwanza kama timu,” alisema Mgunda. Nabi kwa upande wake alisisitiza wanaenda Sudan wakiwa na kiu moja tu ya kupata matokeo mazuri yatakayowavusha kwenda makundi licha ya kujua haitakuwa kazi rahisi kwa namna Al Hilal ilivyo na rekodi nyumbani na hata ilivyocheza kipindi cha pili kwenye mechi ya kwanza wikiendi iliyopita.
The post Makundi hapa kazi moja tu! appeared first on soka letu.
source https://mjombazecoder.website/57735/

Comments
Post a Comment