MZIZIMA ‘Derby’ imetamatika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa wenyeji Azam FC kushinda bao 1-0 lililofungwa dakika ya 35 ya kipindi cha kwanza na mshambuliaji, Prince Dube. Ushindi huu ni wa kwanza kwa Azam dhidi ya Simba baada ya kupita miaka mitano tangu mara ya mwisho iliposhinda pia bao 1-0, Januari 28, 2017, lililofungwa na John Bocco ambaye kwa sasa ni nahodha kwenye kikosi cha Simba. Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote mbili kushambuliana kwa zamu huku wenyeji Azam wakiendelea kutumia njia Ile Ile ya kushambulia kwa kushtukiza. Dakika ya 60, Azam ilifanya mabadiliko ya kuwatoa Kipre Junior na Kenneth Muguna huku nafasi zao zikichukulia na Idd Suleiman ‘Nado’ na Yahya Zayd ili kuongeza nguvu katika ushambuliaji. Kwa upande wa Simba chini ya Kocha Mkuu, Mgunda alifanya mabadiliko pia dakika ya 65 kwa kumtoa Habib Kyombo ambaye tangu mwanzo hakuwa na mchezo mzuri na nafasi yake ikachukuliwa na nahodha, John Bocco. Simba iliendelea kufanya mabadiliko ambapo iliwatoa Augustine Okrah, Jonas Mkude huku nafasi zao zikichukuliwa na Peter Banda na Kibu Denis kwa lengo la kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji. Kwa upande Azam nao waliendelea kufanya mabadiliko ambapo ilimtoa mfungaji wa bao Prince Dube huku nafasi yake ikichukuliwa na Rodgers Kola wakati Nathaniel Chilambo akiingia pia kuchukua nafasi Ayoub Lyanga. Simba ilifanya tena mabadiliko ya kumtoa kiungo wake Nassoro Kapama huku nafasi yake ikichukuliwa na winga mshambuliaji, Pape Sakho. Licha ya mabadiliko hayo ya kiufundi kwa timu zote ila ni Azam chini ya Kaimu Kocha wake Mkuu, Kali Ongala aliyepewa nafasi hiyo baada ya kuondoka Mfaransa, Denis Lavagne ndiye ambaye amenufaika zaidi na ushindi huu. Kwa matokeo haya yanaifanya Simba kupoteza mchezo wake wa kwanza msimu huu chini ya Juma Mgunda baada ya kuanza vizuri tangu alipochukua mikoba ya Mrsebia, Zoran Maki. Kikosi cha Azam kilichoanza ni Ali Ahamada, Lusajo Mwaikenda, Bruce Kangwa, Daniel Amoah, Edward Manyama, Isah Ndala, Ayoub Lyanga, James Akaminko, Prince Dube, Kenneth Muguna na Kipre Junior. Wachezaji wa akiba ni Wilbol Maseke, Nathaniel Chilambo, Cleophance Mkandala, Yahya Zayd, Tape Edinho, Idd Nado, Rodgers Kola, Abdallah Kheri na Idris Mbombo. Kikosi kamili cha Simba kilichoanza ni Aishi Manula, Erasto Nyoni, Mohamed Hussein ‘Tshabala’, Joash Onyango, Henock Inonga, Jonas Mkude, Clatous Chama, Nassoro Kapama, Habib Kyombo, Moses Phiri na Augustine Okrah. Wachezaji wa akiba ni, Beno Kakolanya, Gadiel Michael, Kennedy Juma, Mohamed Quattara, Victor Akpan, Peter Banda, John Bocco, Kibu Denis na Pape Sakho.
The post Azam FC yavunja rekodi ya ‘Mzizima Derby’ iliyodumu kwa miaka 5 appeared first on soka letu.
source https://mjombazecoder.website/58435/

Comments
Post a Comment