Skip to main content

Dk. Mpango aipa maagizo Wizara ufumbuzi changamoto ya maji Mwanza

Na Clara Matimo, Mwanza

BAADA ya uwepo wa tatizo la uhaba na mgawo wa maji katika Jiji la Mwanza, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango ameiagiza Wizara ya Maji kuongeza uzalishaji kwenye mradi mpya unaojengwa Butimba ili kuipatia ufumbuzi changamoto hiyo.

Dk. Mpango ametoa agizo hilo leo Septemba 14, 2022 jijini hapa baada ya kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa chanzo na kituo cha tiba ya  maji  Butimba kinachojengwa na mkandarasi Ms Sogea Satom kutoka nchini Ufaransa kwa gharama ya Sh bilioni 69.3 akisimamiwa na Mamlaka ya Maji Safi  na Usafi wa Mazingira Mwanza (Mwauwasa) ambao ukikamilika utakua na uwezo wa kuzalisha lita milioni 48 kwa siku na utanufaisha wakazi 450,000.

Baadhi ya viongozi wa serikali pamoja na Chama cha Mapinduzi  (CCM) wakiwa wameketi meza kuu na Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi kwenye ujenzi wa mradi wa chanzo na kituo cha tiba ya maji kilichopo Kata ya Butimba Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza.

Amesema inashangaza kuona wakazi wa jiji hilo wanahangaika na kupata shida ya maji wakati wanakaa kando ya Ziwa Viktoria hivyo akaagiza mradi huo ukamilishwe mapema Desemba mwaka huu badala ya Februari, 2023.

“Kutaneni na mkandarasi mumpe maelekezo mahususi ili ukamilike Desemba mwaka huu na muhakikishe wananchi hawa wanapata maji ya uhakika nikiona mnasua sua nitaamua kuja kulia krismasi hapa Mwanza, msithubutu kunizingua maana kabla sijaenda kwa mama (Rais) mtakuwa mmepata habari yenu.

“Sitakubali kutoa ahadi ya uongo mbele ya wananchi hawa, muwasimamie wakandarasi kweli kweli wafanye kazi usiku na mchana,” alisema Dk. Mpango.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais aliipa maagizo manne Mwauwasa katika kutoa huduma bora kwa wananchi wanaotumia huduma ya maji, ikiwemo kuhakikisha wale wanaoishi karibu na chanzo chicho cha Butimba kupewa kipaumbele wakati wa usambazaji wa maji na waliopata ajira walipwe kwa wakati stahiki zao.

Pia, kutochelewesha huduma ya kuunganisha maji kwenye makazi ya wananchi kwa kuhakikisha huduma hiyo wanaipata ndani ya siku saba, kutowabambikizia wateja wao ankara za maji zisizo na uhalisia huku akiwataka Watanzania waliopata nafasi kwenye mradi huo kuwa waaminifu na kutojihusisha na wizi wa vifaa vya ujenzi.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima amesema makadirio hadi mwishoni mwa mwaka 2021 mahitaji ya maji katika mkoa huo ni lita milioni 160 kwa siku, ambapo chanzo kilichopo cha Capripoint kinazalisha lita milioni 90 hivyo upungufu  uliopo ni lita milioni 70 kwa siku ambao unasababisha Mwauwasa kutoa huduma hiyo kwa mgao hususani katika maeneo ya miinuko mikali na pembezoni mwa jiji.

“Kukamilika kwa mradi huu hakika itakuwa ni faraja kubwa sana kwa wakazi wa mkoa huu tunaendelea kuishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na wewe Makamu wa Rais Dk Mpango kwa kutuletea mradi huu,”amesmea Malima.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ameahidi kulisimamia agizo la Dk. Mpango kwa kuwasimamia wakandarasi wanaojenga mradi huo ili ukamilike ndani ya kipindi alichoelekeza (Desemba mwaka huu) huku akibainisha kuwa katika kutatua changamoto ya upatikanaji maji Serikali imeiwezesha wizara hiyo fedha za kununua mitambo ili kuchimba visima kila mkoa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Antony Sanga alisema mradi huo unatekelezwa kwa fedha za mkopo wa masharti nafuu kutoka Shirika la Maendeleo la Ufaransa(AFD) na benki ya uwekezaji ya Ulaya(EIB) ukilenga kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji katika maeneo ya pembezoni mwa jiji la Mwanza pamoja na maeneo ya wilaya zinazozunguka jiji hilo.

Naye Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula amesema utekelezaji wa ujenzi wa chanzo hicho ambacho ni kikubwa ni hatua nzuri kwa wakazi wa jiji la Mwanza kwani kukamilika kwake kutakuwa mkombozi kwa wakazi wa jimbo lake.

“Imani yetu wakazi wa Nyamagana chanzo hiki kikikamilika tutakuwa tumepona na tena tumepona sana, tunaishukuru Serikali kwani mbali na mradi huu tunao mradi wa soko kuu na stendi ambayo inajengwa ndani ya jimbo letu, miradi hii ikikamilika itakuwa ni vyanzo vikubwa vya mapato vitakavyowasaidia wananchi kupitia halmashauri yao kusukuma miradi mingi ya maendeleo,” amesema Mabula.

The post Dk. Mpango aipa maagizo Wizara ufumbuzi changamoto ya maji Mwanza appeared first on soka letu.

Via soka letu https://ift.tt/wHBMQfr

Comments

Popular posts from this blog

Dr. William Samoei Ruto: muuza kuku ambaye sasa ni rais wa Kenya

Ruto ameweka historia kwa kuwa mgombea wa kwanza wa urais katika Jamhuri ya Kenya kushinda kura za urais katika jaribio la kwanza. Amekuwa naibu wa kwanza wa rais kushinda kiti cha urais katika Jamhuri ya Kenya. Mwanasiasa ambaye hajawahi kushindwa katika uchaguzi wowote. Mwanasiasa ambaye ametajwa na wachambuzi kama mchapa kazi na mwenye bidii na kiu ya kupata kile anacholenga maishani. Mtu asiyekata tamaa. Mcheshi katika hotuba zake, anayesemekana kutaka kujua kila linaloendelea karibu naye, mtu mkarimu mwenye roho ya kuchangisha pesa kwa watu na kwa ajili ya miradi mbalimbali. Ruto ameshutumiwa kwa kashfa kadhaa hasa za ufisadi bila kesi kufikishwa mahakamani, na ameshinda karibu kesi zote ambazo zimewahi kufunguliwa mahakamani dhidi yake ikiwemo kesi katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC. Yafuatayo ndiyo mambo muhimu yanayomhusu rais wa 5 wa Jamhuri ya Kenya Dr. William Samoei Ruto. Majina Kamili: William Samoei Arap Ruto Umri: miaka 55 Mke wake: Rachel Chebet Ruto ...

Jioni

Download Audio The post Jioni appeared first on soka letu . source https://mjombazecoder.website/54168/

Bunge la Somalia limemchagua tena Rais wa zamani Hassan Sheikh Mohamud kuwa rais ajaye

Bunge la Somalia limemchagua tena Rais wa zamani Hassan Sheikh Mohamud kufuatia upigaji kura uliofanyika Jumapili mjini Mogadishu. Upigaji kura huo ulifanyika katika uwanja wa ndege wa Mogadishu uliokuwa na ulinzi mkali huku wanajeshi wa Umoja wa Afrika wakilinda hema la Afisyone ambalo lilikuwa ni sehemu ya kupigia kura. Katika kikao cha pamoja cha mabaraza mawili ya bunge yenye wajumbe 328 waliwapigia kura wagombea 36 wa urais katika duru tatu. Mohamud alimshinda Rais aliyekuwa madarakani Mohammed Abdullahi Mohamnmed maarufu kama “Farmaajo” katika duru tatu za upigaji kura. Hassan Sheikh Mohamud alikuwa rais kati ya Agosti 2012 na Februari 2017. The post Bunge la Somalia limemchagua tena Rais wa zamani Hassan Sheikh Mohamud kuwa rais ajaye appeared first on soka letu . Via soka letu https://ift.tt/ZmsWCwT