Kupungua au Kukosa Hamu ya Kufanya Mapenzi (Low or Loss of Sexual Libido)
Matatizo ya kukosa au kupungua hamu ya kujamiana yanatambulika kama tatizo linalojirudia kwa muda mrefu ambapo huathiri mzunguko wa tendo la kujamiana (kusisimka, kufikia kilele, kurudia) na hivyo kusababisha msongo wa mawazo au kuharibu uhusiano kati ya mtu na mwenza wake. Katika makala hii, mwandishi wako Dk. Khamis Hassan anachambua vitu vinavyoweza kusababisha tatizo hili na jinsi ya kuliepuka.
Kupungua au kukosa hamu ya kufanya mapenzi ni suala linaloonekana kuathiri wenza wengi. Jamii imeshuhudia visa vingi vinavyosababishwa na mwenza mmoja kutoka nje ya ndoa au uhusiano kwa kisingizio cha kutoridhishwa na utendaji wa mwenzake katika suala la kujamiana. Kadhalika jambo hili limesababisha kuvurugika kwa ndoa nyingi na wakati mwingine kusababisha magonjwa au hata vifo kwa mmoja au wenza wote wawili
Lakini nini hasa sababu ya kuwepo kwake?
Kwa ujumla visababishi vya tatizo hili kwa wanaume na wanawake ni pamoja na msongo wa mawazo uliokithiri. Asilimia kubwa ya ukosefu wa hamu ya kujamiana husababishwa na msongo wa mawazo unaompata mwenza mmojawapo kwa sababu ya ugumu wa maisha (uchumi), matatizo katika uhusiano (ugomvi, kutoelewana, kutoaminiana au kukosa uaminifu katika uhusiano {infidelity} n.k) au magonjwa mbalimbali. Sababu nyingine ni kupungua au kukosekana upendo/mapenzi katika uhusiano/ndoa, unywaji pombe kupindukia, na utumiaji wa dawa za kulevya.
Aidha kujifungua mtoto nako kunaelezwa kuwa ni chanzo kingine cha kuwepo kwa tatizo hili kwa wanawake. Hii inatokana na ukweli kuwa, mama anaponyonyesha, homoni aina ya prolactin huwa katika kiwango cha juu. Pamoja na kazi nyingine za Prolactin, homoni hii pia humfanya mtu kuridhika baada ya kujamiana (sexual refractory period) kwa kuingiliana na ufanyaji kazi wa homoni nyingine ya dopamine ambayo humfanya mtu kufikia kilele.
Sababu nyingine ni kupungua kwa mzunguko wa damu katika sehemu za siri za mwanamke na hivyo kumsababishia maumivu wakati wa kujamiana, na kwa wanawake wenye matatizo ya homoni ya tezi la thyroid yajulikanayo kama hypothyroidism hupatwa na tatizo hili zaidi kuliko wanaume. Wapo baadhi ya wanawake wanaokumbwa na tatizo la vaginismus ambalo husababisha sehemu za siri za mwanamke kuwa ndogo wakati wa kujamiana na hivyo kumsababishia maumivu makali na kumfanya akose hamu ya kujamiana tena.
Comments
Post a Comment