Aidha utumiaji wa vidonge vya kupanga uzazi au vya majira kwa muda mrefu (kwa wanawake), ugonjwa wa kisukari (wa wanaume na wanawake), uzito uliopitiliza (obesity) pamoja ugonjwa wa viungo vya mifupa yaani arthritis navyo vinaelezwa kuwa chanzo cha kuwepo kwa tatizo hili.
Ujauzito pia unaelezwa kuwa sababu nyingine ya baadhi ya wanawake kukosa hamu ya kujamiana. Hii inatokana na kuwepo kwa mabadiliko katika mfumo wa homoni na maumbile ya wanawake wakati wa ujauzito, hali inayowafanya baadhi ya wanawake kutojiamini.
Wanawake waliowahi kufanyiwa upasuaji wa kuondoa mfuko wa uzazi (hysterectomy) na kusababisha madhara katika neva inayohusika na kuongeza msisimko wakati wa kujamiana (pudendal nerve damage) huwa katika hatari ya kupata tatizo hili. Madhara ya neva hii pia huonekana hata kwa wanaume.
Visababishi vingine ni pamoja na madhara yatokanayo na matumizi ya baadhi ya dawa kama vile za kutibu shinikizo la damu (antihypertensives), msongo wa mawazo (antidepressants) na saratani; kuwa na ugonjwa wa moyo, saratani ya aina yoyote ile, au kuwa na wasiwasi (anxiety).
Kwa wanawake, uchovu unaotokana na kuzidiwa na majukumu ya kulea mtoto/watoto, kazi na kumhudumia mume wake nao unaweza kuchangia kukosa hamu ya kujamiana. Aidha mwanamke mwenye historia ya kubakwa, au aliyewahi kupata maumivu wakati wa kujamiana siku za awali kutokana na kutokuwa tayari kujamiana au kutotayarishwa vyema naye pia ana hatari ya kukumbwa na tatizo hili.
Kupenda mtandao (internet) kupita kiasi (internet addiction) nako kumeelezwa kuwa sababu nyingine ya kuwafanya wenza kukosa hamu ya kujamiana. Kwa mujibu wa utafiti mmoja uliofanyika mwaka 2011 huko nchini Marekani, ilionekana kwamba kati ya ndoa 6,000 zilizovunjika, asilimia 57 ya ndoa hizo zilisababishwa na mwenza mmoja au wote wawili kupenda kuchat au kutumia mtandao kupita kiasi na hivyo kusababisha kupotea kwa msisimko kati ya wenza na hatimaye kupungua uwezo au hamu ya kujamiana.
Uvutaji sigara ni chanzo kingine cha kukosa au kupungua hamu ya kujamiana na huathiri wote wanaume pamoja na wanawake. Uvutaji sigara hupunguza vichocheo aina ya testerone kwa wanaume, na kitendo cha kuwa na kiwango kidogo cha homoni hii husababisha wavutaji sigara wengi kupata tatizo la kupungukiwa uwezo wa kujamiana. Kadhalika uvutaji sigara hupunguza mzunguko wa damu unaopita kwenye uume hivyo kumfanya muhusika kushindwa kusimika au jongoo kushindwa kupanda mtungi (vascular impotence) na hatimaye kukosa uwezo wa kujamiana. Kwa wanaume, uvutaji sigara hupunguza kiwango na uzito wa shahawa (concentration of spermatozoa in semen) kwa takribani asilimia 22-57, wakati uwezo wa mbegu za kiume kuogelea kufikia mirija ya uzazi ya mwanamke nao pia hupungua kwa asilimia 20 ikilinganishwa na wasiovuta. Aidha tafiti kadhaa zimethibitisha uvutaji sigara unaweza kusababisha kuzalishwa kwa mbegu za kiume zisizo na maumbile ya kawaida hivyo kuongeza uwezekano wa kuharibika kwa mimba itakayotungwa (spontaneous abortion) au kuzaliwa kwa mtoto mwenye hitilafu za kimaumbile (birth defects). Pia uvutaji sigara uharibu mirija ya seminiferous tubules (sehemu ambapo mbegu za kiume hutengenezwa) iliyopo kwenye korodani na hivyo hupunguza wingi na uzito wa mbegu hizo. Mambo haya huweza kumfanya mwanaume ajihisi aibu kufanya mapenzi na mwenza wake hali ambayo ikiendelea kwa muda mrefu huwa sugu na kusabsbisha kukosa hamu ya kujamiana moja kwa moja.
Sababu nyingine ni pamoja na umri kuwa mkubwa. Wanaume wenye umri wa kuanzia miaka 40 huwa na ongezeko kubwa la kiwango cha homoni ya prolactin ambayo husababisha kuongezeka kwa kichocheo kingine cha dihydro-testerone inayosababisha kuvimba kwa tezi dume hatimaye kupunguza uwezo wa kusimika kwa mwanaume, na mwishowe kukosa au kupungua hamu ya kujamiana.
Comments
Post a Comment